top of page

Karatasi ya Taarifa ya Mshiriki na Fomu ya Idhini

Fomu hii ya Idhini yenye Taarifa ina sehemu mbili:

  1. Karatasi ya Taarifa 

  2. Cheti cha Idhini

 

Unaweza kupakua fomu hii au kuomba nakala yako kwa kutuma barua pepe kwenye kenya-study@nivi.io.

 

Sehemu ya 1:Karatasi ya Taarifa

 

Kwa nini mradi huu ni muhimu?

Tunakualika kushiriki katika utafiti kuhusu afya ya wanawake. Madhumuni ya utafiti huu ni kuelewa jinsi askNivi inawasaidia wanawake kama wewe kupata huduma muhimu za afya. Utafiti huu ni ushirikiano kati ya AskNivi Limited na mpelelezi kutoka chuo kikuu cha Moi.

 

Nani anaweza kushiriki katika utafiti huu?

Tunatafuta wanawake wenye umri kati ya miaka 18 hadi 29 wanaotumia WhatsApp, ni wapya kwenye askNivi, wanajua kusoma na kuandika kwa Kiingereza au Kiswahili, wapo kwenye uhusiano wa kimapenzi, hawana mimba, kwa sasa hawatumii njia zozote za kisasa za uzazi wa mpango, wanataka kuchelewesha au kuzuia mimba kwa miaka 2 au zaidi, na wanaishi sehemu zilizo na umbali wa kilomita 10 kutoka kwa mtoa huduma wa kupanga uzazi katika hifadhidata yetu.

 

Kushiriki kwa hiari

Ukiamua kushiriki katika utafiti huu wa hiari, utajiunga na hadi wanawake wengine 1000 ambao pia wataamua kushiriki. Unaweza acha kushiriki wakati wowote bila adhabu.

 

Utafiti huu utaendelea kwa muda gani?

Utafiti utachukua takriban mwezi mmoja.


 

Je, ni nini kinachohusika katika utafiti huu?

Tutakuomba ujibu baadhi ya maswali kuhusu afya na mahusiano yako leo, na tutakufuatalia nawe (pia kupitia WhatsApp) baada ya mwezi mmoja. Maswali haya ni mafupi na yatachukua takriban dakika 5-10 tu za muda wako kukamilisha.

 

Kila mwanamke anayejiandikisha katika utafiti ataalikwa kujaribu askNivi bila malipo. Maudhui unayoona yanaweza kuwa kuhusu kupanga uzazi, afya ya hedhi, au mada nyinginezo ambazo mara nyingi wanawake wa umri wako hutuuliza kuzihusu. Seti ya maudhui unayoona itakuwa ya nasibu.   

 

Iwapo mabadiliko yatafanywa kwenye utafiti au taarifa mpya itapatikana, utafahamishwa.

 

Kuna hatari gani?

Hatutarajii kuwa utakabiliwa na hatari au usumbufu wowote ukiamua kushiriki. Tutakuuliza maswali kadhaa kuhusu afya yako na mahusiano, lakini uko huru kujibu kila wakati. Kumbuka, unaweza pia kuacha kushiriki wakati wowote bila adhabu. Hatari moja ya kuzingatia ni uwezekano mdogo kwamba maelezo unayoshiriki nasi hayatabaki kuwa ya faragha.

 

Je, tutalindaje maelezo yako na kudumisha usiri?

Tunafanya kazi kwa bidii ili kuweka maelezo yako salama na ya siri, lakini programu za kidijitali kama vile askNivi haziwezi kutoa hakikisho. Kuna sababu kadhaa za kujifahamu kuwa uko salama katika maingiliano yako na sisi, hata hivyo.

  • Kwanza, ujumbe unaotutumia kupitia WhatsApp umesimbwa kwa njia fiche. Hakuna anayesoma jumbe zako anaposafiri kutoka kwako hadi kwenye seva za WhatsApp na hatimaye kuja kwetu. 

  • Pili, ujumbe unapotufikia, tunauhifadhi kwenye hifadhidata salama. 

  • Tatu, WhatsApp hukupa udhibiti wa ujumbe wako. Njia mbili unazoweza kuimarisha usalama upande wako ni a) kusanidi kifunga skrini kwa simu yako na b) kuwasha kipengele cha kufunga skrini kwa WhatsApp (jua aje hapa).WhatsApp pia hukuruhusu kufunga mazungumzo yako nasi, au uyafute kabisa.

 

Je, ni faida gani?

Hakuna faida za moja kwa moja za kushiriki katika utafiti huu ambazo ni tofauti na kuchagua kutumia askNivi nje ya utafiti.

 

Fidia

Ukiamua kushiriki, hata hivyo, tutakufidia kwa muda na juhudi zako. Unaweza kupata Ksh 600 kwa kujibu maswali leo, na Ksh 600 nyingine kwa kujibu maswali yetu ya kufuatilia baada ya mwezi mmoja. Tutatuma motisha zote mbili kwa simu yako ya rununu.

 

Nini kitatokea kwa matokeo?

Kabla ya uchanganuzi, tutakusanya data kutoka kwa kila mtu anayejiandikisha katika utafiti na kuondoa taarifa zozote zinazokutambulisha kama mtu binafsi. Seti hii ya data isiyojulikana itatumika kwa uchanganuzi na itashirikiwa na watafiti wengine ili kukuza uwazi katika utafiti na utumiaji upya wa data. Maelezo kama vile jina na nambari yako ya simu HAITAshirikiwa kamwe na mtu yeyote. Data isiyojulikana itaonekana kama hii:

Unaweza kuomba nakala ya ripoti zozote za utafiti zinazotoka katika kazi hii kwa kutuandikia katika kenya-study@nivi.io. Tutafurahi kukupa matokeo.

 

Ninaweza kuwasiliana na nani?

 

Ikiwa una maswali yoyote ambayo ungependa kujadili kabla ya kuamua kujiandikisha katika utafiti, unaweza kurudi kwa WhatsApp na uonyeshe hili; mtu kwenye timu atawasiliana nawe. Kama una maswali yoyote baada ya kujiandikisha, unaweza tuma barua pepe kwal Dr. Eric Green kwenye kenya-study@nivi.io ama kupiga simu kwa Dr. Violet Naanyu kwenye nambari +254710952029.

 

Ikiwa una maswali kuhusu haki zako kama somo la utafiti, unaweza kuwasiliana na:

 

The Secretary ESRC

Amref Health Africa in Kenya

Wilson Airport, Lang’ata Road

Simu ya Ofisi:  +254 20 6994000

Simu ya Rununu: 0795746777

Faksi: +254 20 606340

Sanduku La Posta: 30125-00100

Nairobi, Kenya


 

Sehemu ya 2: Cheti cha Idhini

 

Tafadhali rudi kwenye gumzo letu la WhatsApp. Hapo utaweza kukubali kushiriki katika utafiti, kukataa kushiriki, au kutujulisha una swali kabla ya kuamua kushiriki.

bottom of page